Header Ads

MBAO YAENDELEA KUPOKEA VICHAPO MECHI ZA KUJIPIMA NGUVU.

 
Klabu ya Mbao bado haijakaa vizuri baada ya kuchezea vichapo viwili mfululizo kwenye mechi za kujipima nguvu iliyocheza hivi karibuni.
Timu hiyo yenye maskani yake Sabasaba wilayani Ilemela jijini
Mwanza, imeweka kambi yake katika Chuo cha Ualimu Butimba mkoani hapa ikijiandaa na Ligi Kuu Bara.
Mbao ilianza kuwajaribu wachezaji wake Jumamosi ya wiki iliyopita kwa kucheza na Mwadui na kumaliza mtanange huo kwa kisago cha mabao 3-1.
Kama haitoshi,wakata Mbao hao wa jijini hapa walirudi uwanjani tena Jumapili kuwakabili Pamba FC inayojiandaa na Ligi Daraja la kwanza na kuambulia kichapo cha mabao 2-0.
Kutokana na hali hiyo, Kocha wa Makipa wa Mbao FC, Soud Slim alisema matokeo hayo hayawezi kuwapa presha au kuwakatisha tamaa na kwamba timu yao ni nzuri.
Alisema kuwa wao kama benchi la ufundi kwa sasa wanahitaji kutengeneza kombinesheni, hivyo suala la matokeo kwenye mechi za kirafiki si kipaumbele.
“Kumbuka hapa tunajaribu mitambo tu, hatuangalii wala kutafuta matokeo, tunataka kutengeneza kombinesheni ya wachezaji na kuona wapi turekebishe,” alisema Slim.
Aliwataka wadau na mashabiki wa timu hiyo na Mkoa kwa ujumla kuwa na subra na kusema kuwa Mbao itakuwa timu bora na yenye ushindani tofauti na msimu uliopita.

No comments

Powered by Blogger.