Header Ads

SHAIRI: LEO NI KUMBUKUMBU YA KUZALIWA KWA SHUJAA HUYU....






































HONGERA OMARY ZONGO
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Busara kama urithi, hekima zako azizi,
Adili umezirithi, ajabu chako kizazi,
Napenda zako hadithi, Zinaishi Simulizi,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Shujaa kama Omar, jasiri mithili Zongo,
Imara kama Jabar, hifadhi kama ya pango,
Bongoni wewe tajir, duniani una lengo,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Msafi wa matamshi, maneno yako nadhifu,
Msafi wa maandishi, swahihi yalo angafu,
Hakika wewe mtashi, ngangari na maarufu,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yako Peponi.

Karima analo kusudi, kukushusha aridhini,
Tena ongeza juhudi, tia mbolea bongoni,
Zidisha vuta nyiradi, imani jaza Moyoni,
Hongera Ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Siku yako kuzaliwa, kumbukumbu Kumbukizi,
Miongo imeshaliwa, ijapo kama majuzi,
Salamu umetumiwa, kongole nazo pongezi,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Mola kakupa kipaji, kipaji kama bahari,
Bahari na yake maji, maji yaliyo na kheri,
Kheri za usimuliaji, usimuliaji mzuri,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Simulizi Zinaishi, nasi tunaishi nazo,
Utamu wake haushi, kila siku jipya wazo,
Mali fasihi andishi, Zongo Omary unazo,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Ndondondo siyo chururu, mwanakwetu Mwanagenzi,
Moyo uupe Uhuru, imani iwe ulinzi,
Katu isiwe udhuru, utu bora ni mapenzi,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Uzidi shika hatamu, magharibi mashariki,
Salama hadi Kiyamu, imani kwako ibaki,
Udumishe Isilamu, kwa njia ilo ya haki,
Hongera ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi

Lenye mwanzo lina mwisho, marefu huwa na ncha,
Iwe leo iwe kesho, hakuchi hadi kukicha,
Baridi hata kwa jasho, swala usije kuacha,
Hongera Ka'kangu Zongo, makazi yawe Peponi.

Na Shablil President
Wa Nyamwezi Kingdom
2017 Kamilishamalengo
0718526159/0763902318

1 comment:

Powered by Blogger.