Header Ads

AJIBU, TSHISHIMBI WAANDALIWA KUIUA NJOMBE MJI

Image result for AJIBU NA TSHISHIMBI


KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amerejea na nguvu mpya ndani ya kikosi hicho, baada ya jana kuwahenyesha vilivyo nyota wa kikosi hicho, akiwamo Ibrahim Ajib, katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Lwandamina, ambaye alikuwa Zambia kwenye msiba wa baba yake mzazi, jana alionekana kuwapa mazoezi ya tofauti wachezaji wake katika kuwajenga kwenye pumzi na stamina.

Katika mazoezi hayo, Lwandamina alianza programu yake kwa kuwapa mazoezi mepesi wachezaji wake, kisha kuwagawa kwenye makundi matatu kwaajili ya kuwapa mbinu mpya zitakazowasaidia kwenye mechi zijazo.

Makundi hayo yalikuwa yanachezea mpira uwanjani na kukabana, huku kundi lililobaki likikimbia mbio fupi wakiwa na mpira, zoezi ambalo lilidumu zaidi ya masaa mawili.

Zoezi hilo lililenga zaidi kuwajenga wachezaji hao katika suala nzima la kuwa na nguvu za kutosha na stamina kabla ya kuwavaa Njombe Mji kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wikiendi hii.

Wachezaji wa Yanga, walionekana kulimudu vema dakika za mwanzo zoezi hilo, lakini kadri muda ulivyokuwa unakwenda walionekana kuelemewa na kasi ya Mzambia huyo.

Katika kuonyesha kwamba hataki utani, Lwandamina hakuwapa nafasi wachezaji hao kupumzika, jambo lililowafanya nyota hao kuelemewa na zoezi hilo.

Baadhi ya nyota walioonyesha kuelemewa na zoezi hilo, mbali ya Ajib, ni Papy Kabamba Tshishimbi na Raphael Daud, ambao mara kadhaa walionekana wakionyesha ishara ya kuchoka, jambo lililomfanya Lwandamina kutaja majina yao mara kadhaa kuwataka kutofanya uzembe katika hilo.

Kwa upande wake, kuna muda Ajib alitoka uwanjani na kukaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba, hali iliyomfanya Lwandamina kumpigia kelele na kumtaka kurejea uwanjani kuendelea na zoezi jingine.

Tshishimbi na Daudi kila mara walionekana kukaa chini kama si kushika magoti na kuonyesha kuwa zoezi hilo liliwaingia barabara.

No comments

Powered by Blogger.