Header Ads

SHAIRI: MWANAFUNZI WA CHUO ALIYEDISCO KISA UTAMU WA PENZI LA PROFESA

PENZI LA PROFESA
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Hadithi hadithi njoo, eti utamu kolea,
Staff ni Kariakoo, kama shuleni ni Daa,
Porofesa shikamoo, penzi lako lanikolea,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Stori ilianzia lekcha, tangia mwaka wa kwanza,
Nilipomuita ticha, kumbe ajua kufunza,
Macho nikayapikicha, kidole kikawa funza,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Quiz aloitoa, mimi simo darasani,
Hofu ikaniingia, nikaenda ofisini,
Goti nikampigia, pate maksi kilaini,
Tamu poenzi la profesa, limefanya nimedisco.

Mwenyewe kanifukuza, hataki hata niona,
Machozi nikajiliza, mwenyewe huku kanuna,
Mafua kuyapuliza, huruma pate iona,
Tamu penzi la profesa,limefanya nimedisco.

Mara katoa kauli, nenda uje baadaye,
Nikahisi ni kivuli, mwanga uje ung'aye,
Nikasema afadhali, kumbe ni kajiandaye,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Muda nao kawadia, nikaenda ofisini,
Miwani akaivua, kalamu kaweka chini,
Nataka kusaidia, kwa pozi na umakini,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.
  
Kama unataka maksi, mimi nataka mapenzi,
Wala siwe wasiwasi, ntakulinda ntakuenzi,
Pesa tele kwa nafasi, nitakupa nalo Benzi,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Moyo kajawa tamaa, kawa sitaki nataka,
Akili ilikataa, huku moyo ukataka,
Neno zito nikatoa, profesa akaniteka,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Na vile sinaga bumu, kwangu ikawa neema,
Vile maisha magumu, kwa tabu ninavyosoma,
Nikampenda mwalimu, penzini zama mazima,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Tukaanza kwenda klabu, wikendi hasa usiku,
Tukaanza gonga ulabu, baga piza chipsi kuku,
Kwangu ni mwisho wa tabu, sasa mimi si kapuku,
Tamu penzi la profesa, nimefanya nimedisco.

Nikasahau na shule, kutwa nipo na profesa,
Leo huku kesho kule, tunakula tu anasa,
Nikampa penzi tele, muziki kama darasa,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

 Penzi likaninogea, nikapoteza ramani,
Semista ikapotea, ikafika mitihani,
Shule kaingia doa, nikafeli siamini,
Tamu penzi la profesa, nimefanya nimedisco.

Sasa muda wa aris, moyoni ni tetemeko,
Nikawa na wasiwasi, moyoni mfadhaiko,
Nilihisi mkosi, matokeo nimedisco,
Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Narudi home najuta, kutwa kulia machozi,
Nichotaka nimepata, narudi kwao wazazi,
Nakumbuka ninajuta, hili funzo la kizazi,

Tamu penzi la profesa, limefanya nimedisco.

Na Shablil President
Wa Nyamwezi Kingdom
2017 Kamilishamalengo
0718615269/0763902318

No comments

Powered by Blogger.