KWA NINI TUNAVAA…?
Mwalimu wangu wa shule ya
msingi alinifundisha ya kuwa mahitaji muhimu ya mwanadamu katika maisha yake ni
chakula, malazi na mavazi. Huenda wahenga hawa walotajirika busara, hekima na
adili za kupindukia waliona ni kwa namna gani mavazi yana umuhimu mkubwa katika
maisha ya mwanadamu.
Bila haka mwanagenzi wa
kisiwa cha kiswahili utakubalina nami ya kuwa mavazi yaani nguo ni ishara tosha
kabisa ya busara, hekima na maadili. Hii
ni sababu yangu binafsi, lakini nilijaribu pia kuzungumza na wadau mbalimbali
juu ya suala la uvaaji.
Nilipomuuliza kijana
Abdillah yeye alinijibu kwa mujibu wa Quran Tukufu akasema. Katika Quran tukufu
mathalani surat AL A’raaf (aya ya 26), Allah anasema “Enyi wanaadamu
tumekuteremshieni nguo (mavazi) kwa ajili ya kuficha tupu zenu (kuhifadhi miili
yenu na sehemu za siri) na pia tumekuteremshieni nguo kwa jili ya mapambo, na
vazi la uchamungu ambalo ndio bora kuliko mavazi yote. Hapa sikutia neno zaidi.
Lakini pia nilipata wasaa
na kuzungumza na kijana John Yunde, pia alinijibu kwa mujibu wa biblia kutoka
katika kumbukumbu la Torati ( 22: 5) mwanamke asivae mavazi yampasavyo
mwanaume, wala mwanaume asivae mavazi ya mwanamke, kwa maana kila afanyaye mambo
hayo ni machukizo kwa bwana wake.
Baada ya kupata nukuu
hizo kutoka kwa vijana hao wema, nilijitafakari kwa muda kisha nikawaza na
kuwazua je kwa nini tunavaa? Sasa mwanagenzi fuatana nami ili tujue kwa nini
tunavaa?
Kumbe dhumuni la kuvaa ni
kujisitiri, kusitiri siri zetu, siri zilizobeba aibu na maana kubwa ya uwepo
wetu hapa katika mgongo wa ardhi. Lakini pia nimejifunza ya kuwa kuna taratibu
za uvaaji kumbe watu wa jinsi ya kiume basi wavae kianaume na wale wenye jinsi
ya kike wavae kike kama Mola wetu Mlezi alivyoagiza.
Najaribu kutafakari jinsi
kizazi cha sanaa, kizazi cha nyoka, kizazi cha dotcom kinavyovaa sasa hivi,
yaani hakuna uvaaji wenye kufuata taratibu wala kanuni yoyote ile yaani tunavaa
tu, vile tunavyojisikia. Suala hili lilinipa msukumo na nguvu kuweza kuzungumza
na vijana wenyewe ambao mpira huu wanatupiwa wenyewe. Nilifanya mjadala mfupi
na vijana Rweymam David, Jackline Christopher, Flora Primo, Hawa Makweba na
Omar Mpondi.
Niling;amua kwa vijana
hawa wao wanadai kuwa ni hulka ya kijana mwenyewe, ulimbukeni huku wengine
wakidai kuwa ni athari za utandawazi. Lakini kwa upande mwingine wa shilingi
walikemea vikali uvaaji huu wa kihuni. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni,
kumbe hata mavazi yana mahala pake, yaani kuwa katika kumbi za starehe ama
ufukweni wao wamebariki kuwa yafaa mtu kuvaa kisasa kuvaa hovyo lakini ukiwa
sehemu rasmi basi ni sharti uvae kiheshima, sasa swali ninalobaki nalo ni Je,
mwili wa mwanadamu kuna maeneo unatakiwa kuhifadhiwa wakati sehemu nyingine
uadhirishwe?
Suala la uvaaji wa
mlegezo yaani kuteremsha suruali mahala ambapo si pake huo ni uhuni usiovumilika,
tena haupaswi kuvumiliwa hata kwa nukta moja ya muda. Hili ni suala baya sana
kwani tunakiuka maagizo ya Mwenyezi Mungu juu ya suala la kujisitiri kusitiri
mwili.
Lakini je vipi kuhusu hawa mabinti wanaovaa
sketi ama gauni fupi, huu pia ni ugonjwa ambao unapaswa kupingwa na kila nafsi
inayoishi katika sayari hii ya tatu.
Tunapokiuka kanuni za
uvaaji tujue kabisa ni kujishushia heshima, ni utovu wa nidhamu na ni
maandilizi ya kujenga kizazi kilichopotea, hivyo nitoe shime kwa kila kiumbe
mwenye kuitwa binadamu na mwenye akili timamu aweze kulipinga suala hili.
Turejee katika maadili ya
uvaaji mzuri, pia suala la kubadilishana mavazi, huyu wa kiume avae ya kike na
wa kike avae ya kiume hii si sawa hata kidogo. Suala la kwenda na wakati si
uvaaji mbovu, si kubadili taratibu za mavazi. Ni kujisitiri mwili. Tusisingizie
joto au mazingira tukumbuke lengo la kuvaa ni nini? kama tutapuuzia haya basi
hatutakuwa tofauti na wanyama ambao hawana habari na mavazi.
Hakuna marefu yasiyo na
ncha, basi nami nisiseme sana, haya kwa leo yanatosha. Waswahili tunasema
mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio haambiwi sikia. Bila shaka
tumesikia lakini mja ni kunena muungwana ni vitendo hivyo tuchukue haya
tuyabebe vifuani mwetu tuyafanyie kazi ili tuweze kurejea lengo la kuvaa.
No comments