Header Ads

KUELEKEA MCHEZO WA WATANI WA JADI KESHO, ULINZI WAIMARISHWA TAIFA.

Image result for MASHABIKI WA YANGA

POLISI 300 wanatarajiwa kuimarisha ulinzi na usalama wa mashabiki uwanjani wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii, utakaowakutanisha vigogo Simba na Yanga kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema polisi hao ni pamoja na wale wanaotumia farasi na mbwa kwa ajili ya kulinda usalama wa watu na mali zao.

“Mechi itachezwa Jumatano (kesho) kuanzia saa 11 jioni lakini milango itafunguliwa kuanzia saa tatu asubuhi, tunaamini usalama utakuwa wa kutosha hivyo tunaomba wadau watakaojitokeza kushuhudia mchezo huo wafuate taratibu zote,” alisema Lucas.

Mgeni rasmi katika mchezo huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye tayari ameandikiwa barua ya mwaliko lakini bado hawajapata uthibitisho wake.

Lucas aliongeza kuwa mbali na mechi ya Simba na Yanga, kutakuwa na ufunguzi wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana wa chini ya miaka 17 (Afcon), zitakazofanyika mwaka 2019, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

“Kabla ya mechi hiyo, Rais wa TFF, Wallace Karia, atazindua michuano ya Afcon kwa vijana ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji na pia kutakuwa na mechi ya maveterani wa Simba na Yanga kwa ajili ya kupamba shughuli hiyo,” alisema Lucas.

No comments

Powered by Blogger.