Header Ads

NIYONZIMA, OKWI, AJIB, TSHISHIMBI WATAPAMBANA NA HALI ZAO KESH

HATIMAYE ile siku ambayo wapenzi wa soka nchini walikuwa wakiisubiri kwa hamu kupima ubora wa vikosi vya Simba na Yanga, inawadia kesho, wakati watani wa jadi hao watakaposhuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa Ngao ya Jamii.


Tayari mwamuzi wa mtanange huo ameshafahamika, ambaye si mwingine, bali ni mwamuzi bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Elly Sassi wa Dar es Salaam.

Tangu mchakato wa usajili wa msimu huu ulipoanza miezi miwili iliyopita, mashabiki wa klabu hizo kongwe walikuwa wakitambiana kwa kila upande kudai kuwa wamesajili vifaa hasa vitakavyowawezesha kutamba msimu huu.

Wakati Simba wakitamba kuwanasa wachezaji nyota kama Haruna Niyonzima aliyetokea Yanga, Emmanuel Okwi ambaye ni mchezaji wao wa zamani aliyerejea Msimbazi baada ya msimu uliopita kukipiga akiwa na SC Villa ya nchini kwao Uganda pamoja na Shomari Kapombe, John Bocco, Erasto Nyoni na Aishi Manula (wote Azam), mshambuliaji Mghana, Nicholas Gyan na wengineo, watani wao hao wamekuwa wakiwabeza kwamba wamesajili wachezaji kwa sifa bila kuangalia mahitaji ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao.

Yanga wao wamekuwa wakidai kuwa pamoja na kusajili wachezaji wachache, wamezingatia zaidi kasoro zilizopo kikosini mwao, wakitolea mfano beki namba tatu wakiwa wamemsajili Gadiel Michael kutoka Azam, kiungo mkabaji (Pappy Kabamba Tshishimbi-DRC), kipa (Youthe Rostand (African Lyon), kiungo mchezeshaji kuziba nafasi ya Niyonzima (Rafael Daudi-Mbeya City) na mshambuliaji mbunifu na fundi wa mpira (Ibrahim Ajib-Simba).

Tayari wachezaji hao wapya wameungana na wenzao katika maandalizi ya msimu mpya, huku wakiwa wameshajinadi kwa mashabiki na viongozi wa timu zao mpya kupitia mechi kadhaa za kirafiki.

Na wakati timu hizo zikishuka dimbani kesho, mashabiki wa kila upande wameonekana kuusubiri mchezo huo kwa usongo wa aina yake, kila upande ukiwa na matumaini ya kikosi chao kushinda kutokana na kile wanachoamini ubora wa usajili waliofanya msimu huu.

Ikumbukwe kuwa, mchezo huo wa kesho ni ishara ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa 2017/18 na kwamba pamoja na azma ya kutwaa ngao hiyo, lakini kila timu itautumia mchezo huo kupima ubora wa usajili wake wa msimu huu na kikosi kwa ujumla.

Lakini wakati mashabiki wa timu hizo wakionekana kuusubiri kwa hamu mchezo wa kesho, kwa wachezaji hali ni tofauti, ambapo wengi wao, hasa wale wapya, watakuwa wakiumiza vichwa vyao jinsi ya kuwakonga nyoyo wapenzi wa timu zao hizo.

Na wachezaji ambao ni wazi watatakiwa kupambana na hali zao kesho, ni wale waliosajiliwa kwa mbwembwe kama Niyonzima, Okwi, Manula, Bocco, Nyoni, Gyan, Jamal Mwambeleko (Simba); Rostand, Gadiel, Tshishimbi, Rafael na Ajib (Yanga).

Kati yao, yeyote ambaye ataamka vibaya kesho na kushindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa na wengi, anaweza kujikuta akiwa katika wakati mgumu kuwaaminisha mashabiki wa timu yake kama alistahili kusajiliwa na klabu zao.

Lakini pia, ifahamike kuwa, kuna wachezaji (wapya) ambao wanaweza wasicheze vizuri kesho, lakini katika mechi zinazofuata za ligi, wakaibuka na kuwa tishio kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, ambaye katika mechi zake za kwanza alionekana kichekesho, kabla ya kuwa moto wa kuotea mbali kwa mabeki na makipa wa timu pinzani.

Yote kwa yote, mashabiki kesho watarajie burudani ya aina yake, lakini iwapo mwamuzi atachezesha kwa kufuata sheria zote 17 za soka, ili kuwawezesha wachezaji kuonyesha kile walichojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

No comments

Powered by Blogger.