NYUMA YA PAZIA: MO MASHINE…
Soka ni mchezo unaochezwa
hadharani yaani kila mtu anaushuhudia. Lakini katika mchezo huu kuna mambo
mengi hujitokeza na ndiyo mambo haya ambayo hufanywa na wachezaji kwa kiasi
kikubwa huwafanya wachezaji hao kujulikana na kuwa na majina makubwa.
Lakini kama ilivyo
kipengele hiki cha nyuma ya pazia hiki huangazia zaidi pale ambapo upeo wa
macho ya mwanadamu haufiki kirahisi. Na leo umekuja kumuangazia kiungo
mshambuliaji wa Simba Mohamed Ibrahim.
Mchezaji huyu huwa
hasemwi sana na vyombo vya habari hata watu wenyewe huwa hawamsemi sana. Labda
jambo hili ndilo humfanya hata kocha kutowaza kumuanzisha katika mechi muhimu
kinyume chake humuacha nje katika benchi asubiri timu izidiwe ndiyo aingie kama
mkombozi.
Kila shetani na mbuyu
wake hivyo huenda mbuyu wa Mohamed Ibrahim Cabaye ukipenda muite MO ni kuanzia
benchi. Moja kati ya wachezaji muhimu kabisa katika klabu ya Simba ni MO ndiyo
maana hata kipindi Ibrahim Ajib anahama timu basi mashabiki na wapenzi wa Simba
walijinasibu kwa kusema “Ajib yeye aende
tu, tunaye MO”.
Kijana huyu aliyesajiliwa
kutokea Mtibwa Sukari ya Manungu Tuliani Morogoro, anavalia jezi nambari 4,
iliyokuwa ikavaliwa na Hassan Kessy aliyehamia Yanga huku yeye akitua hapo na
kuichukua mwanzoni mwa msimu uliopita.
Tangu ametua Simba
amekuwa katika kiwango cha hali ya juu kitu kinachomfanya sasa kuonekana kama
mkombozi wa timu pale inapozidiwa utasikie “muingize
MO ndani”. Kauli hizi si za utani bali ni uhalisia kwa kijana huyu ambaye kila
akicheza mathalani kwa kutokea benchi amekuwa akifanya makubwa na kugeuka lulu
ya Msimbazi.
Labda nukukumbushe
michezo kadhaa ambayo amekuwa akicheza mara nyingi amekuwa akienda kupindua matokea
na muda mwingine akifunga yeye mwenyewe. Kuna wakati aliumia na pengo lake likaonekana.
Mchezo wa kwanza
ninaotaka tuuzungumzie ni ule wa nusu fainali kati ya Simba na Azam uliochezwa
uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kumalizika kwa Simba kushinda kwa goli
1 – 0. Goli pekee katika mchezo huo lilifungwa na Mohamed Ibrahim MO CABAYE
dakika chache kabla hajalimwa kadi ya njano ya pili na mwamuzi kuamua kumtoa
nje kwa kadi nyekundu. Licha ya kutolewa kwa kadi nyekundu lakini goli lake
lilidumu na kuifanya Simba kutinga fainali na hatimaye kuibuka bingwa wa kombe
la FA, hivyo kukata kiu yao ya vikombe lakini pia kuweza kukata tiketi ya
kushiriki michuano ya kimataifa ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Tarehe 8 Agosti mwaka huu
Simba ilishuka dimbani kumenyana na klabu ya soka ya Rayon Sports ya Rwanda
siku ya kilele cha maadhimisho ya Simba Day. Mchezo huo ambao hutumika
kutambulisha wachezaji mathalani wapya uliochezwa uwanja wa taifa jijini Dar es
salaam, ulimalizika kwa Simba kushinda ushindi mwembamba wa goli 1 – 0. Goli
pekee likifungwa na Mohamed Ibrahim MO CABAYE. Kutoakana na usajili uliofanya
na klabu hiyo mwaka huu ingekuwa aibu kubwa sana kwenda suluhu na bingwa hao wa
Rwanda, si kwa sababu Rayon hawajui mpira la hasha, bali ni kutokana na tambo
na mbwebwe za mashabiki wa Simba. Na goli hilo la MO lilitosha kabisa kufuta
aibu hiyo badala yake kuamsha ndelemo vifijo na shamrashamra katika mitaa ya Msimbazi.
Jumatano Agosti 23, 2017,
MO anaingia katika rekodi kubwa ya soka la Tanzania kwa kuiwezesha klabu yake
kuchukua taji la ngao ya jamii. Alipiga penalti ya mwisho kwa ufundi na ustadi
wake na kuifanya Simba kuwa mabingwa. Licha ya kwamba alichelewa kuingia
lakini kiwango chake kilikuwa kizuri cha halio ya juu.
Jambo zuri ni kwamba MO
ameumbika kisoka amestaarabika kiuchezaji hivyo kuwa miongoni mwa lulu za mpira
wetu. Nmamuona MO katika moja ya vilabu vikubwa Ulaya tena katika ligi kubwa na Mwenyezi
Mungu amuwezeshe kutimiza jamabo hili kwani anatashili kabisa bila ya kumung’unya
maneno au kupepesa macho macho.
Kila la kheri MO.
Weka maoni yalo hapa.
No comments