Header Ads

SHAIRI KUHUSU WATOTO WA LUCKY VICENT: MEI SITA YA MAJONZI

Nawasha yangu kurunzi, nianze andika utenzi,
Moyoni nina majonzi, mwili wajawa na ganzi,
Ghafla nashusha pumzi, kumshukuru Mwenyezi,
Ni msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Ghafla simu nafungua, WhatsApp naingia,
Taarifa zaenea, picha za kusisimua,
Ajali imetokea,huko mlima Rhotia,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Gari limetumbukia, wanafunzi limeua,
Thelathini na kadhaa, na walimu wao pia,
Dereva hajabakia, tanzia kote tanzia,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Hao wanafunzi wetu, hao ni watoto wetu,
Hao ni walimu wetu, hao wote ndugu zetu,
Hao ni Kizazi chetu, poleni wana Karatu,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Pole kwa wao wazazi, walojawa na majonzi,
Moyoni tuna simanzi, machoni tuna machozi,
Hiyo kazi ya Mwenyezi, amefanya kwa mapenzi,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Kwa pamoja tunalia, tunalia Tanzania,
Hii kwetu ni tanzia, huzuni imetujaa,
Tuzidi kuwaombea, peponi pakufikia,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Tunapita hii dunia, hakuna ato bakia,
Wao wametangulia, sisi tutawafuatia,
Kikubwa kujiandaa, kwa Mola kutubia,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Walichanua maua, wamezima kama taa,
Kifo mlango ni njia, sote tutaupitia,
Kikubwa kujiandaa, ibada zenye kufaa,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Lucky Vicent simanzi, kupoteza wanafunzi,
Tuliwapa na mapenzi, pamoja bora malezi,
Kwarudisha hatuwezi, tumshukuru Mwenyezi,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

Mwisho nizitoe pole, kwake mkuu wa shule,
Wazazi watoto wale, watanzania pia pole,
Njia yetu ile ile, hatutoishi milele,
Huu msiba wa taifa, mei sita ya majonzi.

 Na Shaaban Maulidi
0718526159

No comments

Powered by Blogger.