Header Ads

SOMA SHAIRI LA KAZI HAPA...KWA ELIMU NA BURUDANI

SHAABAN PIGA KAZI
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Shaaban piga kazi, piga tu kazi mwanangu,
Wala sichague kazi, riziki atoa Mungu,
Juhudi katika kazi, usifate walimwengu,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Bongo bahati mbaya, hiyo kauli ni Liya,
Bongo yako himaya, usije kuikimbiya,
Wala siwaze Ulaya, Bongo ndiyo yako kaya,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi

Kazi kuchoma mkaa, ama kushona viatu,
Dobi nguo kuzifua, usiwasikilize watu,
Ama uza vitumbua, maisha kama upatu,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Mchicha lima Bustani, ama matikiti maji,
Sukuma na mkokoteni, ufundi griss gereji,
Nyanya kauze gengeni, ama chimba mifereji,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Wewe piga vibarua, ikibidi seremala,
Mtoni nenda kuvua, ama chimba majalala,
Bodaboda kamatia, ama konda daladala,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Ikibidi kuwa chinga, wa kuuza mitumba,
Ama uuze Karanga, ikibidi lima shamba,
Hata miko kuichonga, ama uwe fundi bomba,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Kazi hata ya ajira, utapata mshahara,
Fanya hata biashara, usifanye masihara,
Shaban cheza mpira, kipaji chako kuchora,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Kazi hata udaktari, shuleni kuwa mwalimu,
Uhasibu ni mzuri, vizuri kuwa Imamu,
Jeshini wewe askari, mahakamani hakimu,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Usisubiri kuajiriwa, mwenyewe kajiajiri,
Usije kurubuniwa, ukaicheza kamari,
Huku unategemewa, Shaban wewe hodari,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Fanya kazi za halali, usifanye za haramu,
Maisha utayabadili, sisikie wanadamu,
Swala kwako muhimili, dunia itakuwa tamu,
Mama yako nimesema, Shaaban piga kazi.

Na Shablil President
Wa Nyamwezi Kingdom
2017 Kamilisha Malengo
0718526159/0718526159

No comments

Powered by Blogger.