Header Ads

SHAIRI: JAMAA ALIYEKOSA MKE KISA DINI...

Image result for ISLAMIC WEDDING CEREMONY
























SABABU NI DINI
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Mapenzi bwana upofu, ukungu ndani machoni,
Mapenzi ukengeufu, sumu ndani ya mboni,
Mapenzi kama uchafu, maji ya taka moyoni,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Ile mapenzi safari, kweli mapenzi ajali,
Hivi mapenzi shubiri, au mapenzi asali?
Hivi mapenzi fakiri, au mapenzi ni mali?
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Mapenzi pata potea, kumbe makosa kosea,
Wewe unapobutua, mimi menikomboa,
Mapenzi mbegu ya ndoa, iweje yawe ni doa?
Eti sababu ni dini Shaban nakosa mke.

Basi mapenzi kidonda, penzi kweli donda ndugu,
Mapenzi kama matunda, mapenzi pia ni mbegu,
Mapenzi sasa yavunda, moyoni naota sugu,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke

Nikampenda Naomi, bint wa mzee Joni,
Yeye awe na mimi, tuzame hadi ndoani,
Nikaukata ulimi, nikamuweka moyoni,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Penzi likawa gizani, mithili ya kombolela,
Tukajibanza tutani, huku viazi tukila,
Hatwonekani nyumbani, hadi muda wa kulala,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Kumbe penzi kikohozi, kulificha hauwezi,
Arobaini si mwezi, ndiyo siku za mwizi,
Mbele yao wazazi, pamoja nao walezi,
Eti Sababu di dini, Shaban nakosa mke.

Tulipanga mimi yeye, sote tuwe dini moja,
Dini abadili yeye, ili tuishi pamoja,
Na kisha wazaziye, wakaja ivunja hoja,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Naomi mkatoliki, baba mzee Kanisa,
Dini nyingine hataki, kuzisikia kabisa,
Mama kawasha fataki, moto unawaka sasa,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.

Wa kwetu wamekataa, wa kwao wamekataa,
Wala hakuna cha ndoa, dini imeleta doa,
Wa kwao wamechagua, kuhama wamekataa,
Eti sababu ni dini, Shaban nakosa mke.


N Shablil President.
Wa Nyamwezi Kingdom.
2017 Kamilishamalengo.
0718526159/0763902318.


No comments

Powered by Blogger.