Header Ads

RUSHWA HAIKUBALIKI
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Rushwa adui wa haki, rushwa haiwi rafiki,
Rushwa kubwa unafiki, rushwa inajenga chuki,
Rushwa yatudhihaki, rushwa haikubaliki,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Mbaya huyu mdudu, kote ametamalaki,
Wala tusimhusudu, tuseme hatutaki,
Katu tusimsujudu, tumuue kwa bunduki,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike.

Mdudu yupo nyumbani, lengo kuivunja ndoa,
Yupo na mahakamani, haki yangu kuchukua,
Yupo pia hospitalini, wagonjwa anawaua,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Ipo na barabarani, yawahadaa trafiki,
Ipo pia bandarini, zipite bidhaa feki,
Rushwa tusiitamani, daima tuidhihaki,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Chanzo chake ni tamaa, haraka ziso haraka,
Hata kama una njaa, rushwa usije itaka,
Puani itakutokea, kinywani kukutapika,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Siyo alama ya Utu, haina ubinadamu,
Siyo mdudu wa kwetu, ni mchungu si mtamu,
Tusiijarabu katu, rushwa mdudu haramu,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Uthamini Utu wako, nakwambia dada yangu,
Usishushe Utu wako, kwa shida za ulimwengu,
Usimpe utu wako, riziki atoa Mungu,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Kama wataka ajira, pita kwenye njia kuu,
Ngono isiwe ujira, boss mtaka makuu,
Rushwa kubwa hasara, tena ni dhambi kuu,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Kwa nini urubuniwe, utu wako ushushiwe?
Huduma uhudumiwe, eti chochote kitowe?
Tena pesa uibiwe, eti ili usaidiwe?
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Zipo nyingi athari, rushwa kuendekeza,
Tena ni kubwa hatari, wengine wawaumiza,
Jaribu kuitafakari, vile watu wawakwaza,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Usidanganywe na pesa, leo ipo kesho huna,
Wengine kuwanyanyasa, kuwafanyia hiyana,
Kina dada nawaasa, msije patwa laana,
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Kwa pamoja tuchukie, rushwa ifike mwisho,
Hatua tuzichukie, jana leo pia kesho,
Mdudu huyu tumuue, abaki ni makumbusho.
Rushwa haikubaliki, chimba shimo tuizike. 

Na Shablil President.
Wa Nyamwezi Kingdom.
2017 Kamilisha Malengo.
0718526159 /0763902318.

No comments

Powered by Blogger.