Rais Buhari asisitiza umoja hotuba ya kwanza baada ya kurejea Nigeria
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameihutubia taifa baada ya kuwa Uingereza kwa miezi mitatu akipata matibabu.
Katika
hotuba yake kwenye televisheni, Buhari, mwenye umri wa miaka 74,
alisema "alifadhaishwa" na wito wa kuigawanya Nigeria, akiwahimiza
Wanigeria kuwa na umoja.
Lakini rais hakufichua anaugua wapi. Hii ilikuwa mara yake ya pili kuchukua likizo kwa sababu za kimatibabu mwaka huu.
Raia wengi wa Nigeria walimwomba ajiuzulu wakati hakuwepo nchini, wakisema hakuwa na uwezo wa kuiongoza nchi.
Wengine wamemuuliza kusema anaugua nini huku uvumi ukiongezeka kuhusu uwezekano wake kuwania urais tena mwaka 2019.
Makamu wa Rais Yemi Osinbajo amekuwa akiwajibika
wakati Buhari amekuwa Uingereza, lakini Buhari sasa amerejelea kazi
yake kama rais.
Akizungumza siku mbili baada ya kurudi kwake,
Buhari alisema kuwa maoni kuhusu kuwaganywa kwa Nigeria "yamevuka mstari
wa rangi nyekundu".
"Umoja wa Nigeria upo na sio wa kujadiliwa," alisema. "Hatuwezi kuruhusu watu wasiowajibika kuleta shida."
Rais pia alizungumzia vita vya kikabila nchini, akisema vinasababishwa na "wahalifu wa kisiasa".
Kuna
watu ambao wamekuwa wakiitisha kuanzishwa kwa nchi tofauti maeneo ya
kusini-mashariki inayojulikana kama Biafra huku vita dhidi ya wanamgambo
wa Kiislamu, Boko Haram vikiendelea katika maeneo ya kaskazini.
Raia wa Nigeria walikuwa wanatumai kupata habari
kuhusu kile kinachomfanya rais wao kuugua lakini ofisi ya rais imekataa
kufichua lolote.
Licha ya kuwa imesisitizwa kuwa Buhari yuko sawa na mwenye afya, alionekana mnyonge akiwasalimia wanasiasa jumamosi.
Ana
nafuu kidogo - mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa mwezi Mei
kabla hajaelekea Uingereza, alipowapokea wasichana 82 wa Chibok
waliokuwa wameachiliwa. Hakuweza kusimama.
Jumatatu alijikakamua
kuonyesha kuwa yuko tayari kuiongoza nchi. Lakini wengi bado wanauliza
maswali kuhusu uwezo wake wa kuiongoza nchi.
Wakati Buhari alikwenda London mara ya kwanza - Juni 2016 - ofisi yake ilisema ni kwa sababu anaugua sikio.
Taarifa
rasmi iliyotolewa mwezi Machi 2017 ilisema kuwa rais amekuwa "kwenye
likizo, na alichukua nafasi hiyo kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu".
Wapinzani wake wakuu katika uchaguzi wa Nigeria wa 2015 walidai alikuwa na saratani ya tezi dume, lakini alikanusha.
No comments