MWANAMKE MWENYE SURA TANO.
Mwanamke ndiyo nguzo ya
familia, nguzo ya jamii, nguzo ya taifa na ni nguzo ya dunia. Ninapotamka
matamshi haya ninakuwa na uhakika na kupata nguvu za kutembea kifua mbele kwani
ninajua kabisa hakuna eneo nililobanmanga maneno.
Sifa za mwanamke zipo
lukiki sana, kila sifa nzuri anayo mwanamke na kila mwanamke anapaswa kujichukulia
kama mwanamke na hana haja ya kupambana kuwa sawa na mwanamke. Kwa sasa naweza
kusema ya kuwa manuari iliyobeba kizazi cha wanawake inaennda mrama. Hii ni kwa
sababu leo wanawake wengi katika sayari pekee hii iliyotunukiwa viumbe hai
ndani mwake wanapambana kuwa wanaume. Inachekesha lakini inasikitisha pia.
Tena zimetokea taasisi,
asasi na mashirika mbalimbali kutoka katika kila kona ya ulimwengu zikidai
zinapambana kuhakikisha wanawake kuwa sawa na wanaume. Mmmh wacha nicheke kwa
kuwa nina kila sababu ya kufanya hivyo, wanawake hawawezi kuwa sawa na wanaume
hilo jambo halipo tena halipo. Halipo kwa sababu mwanamke ni mwanamke na
mwanaume ni mwanaume. Mungu ameumba hivyo nasi tupo hivyo.
Badala ya kuendeleza
mijadala, midahalo, semina ama warsha za kumjengea ghorofa la mawazo na fikra
potofu kuwa mwanamke awe sawa na mwanaume. Kitu ambacho aghalabu ni lulu kwa
sasa ni kuhakikisha kuwa mwanamke anavaa vazi la heshima, vazi takatifu, vazi
ambalo Mola Mlezi amemtabaruku. Na si vazi jingine bali ni vazi la uanamke.
Hilo ndilo haswa linamfaa linamtosha na linampendeza zaidi ya hilo analolitaka
sasa.
Ama kuhusu kichwa cha
Makala hii ni sura tano za mwanamke, hakika mwanamke anazo sura tano kwa
mtazamo wangu lakini ikiwa ni sura nne tu zenye kumpendeza na hiyo moja ni ya
bandia ambayo inamfanya atoke katika taswira ya mwanamke na kubaki katika
kibonzo tu cha mwanmke.
Sura
ya kwanza ni Mwanamke dada. Kila mwanamke anayezaliwa lazima
apitie katika surah ii. Ni sura ambayo huvaliwa punde tu baada ya fikra za mwanadamu
huyu kuwa amepevuka kiakili na kukua kimwili na kuweza kupembua mbichi na
mbivu. Ndiyo haswa buwa kama bawabu itakayompa mtu ruhusa ya kuingia katika
hatua nyingine za makuzi. Katika surah ii mwanamke anapaswa kujifunza kuwa
nadhifu kwa matendo, mawazpo na mavazi kiasi kwamba kuwa kiigizo kwa wadogo
zake, lakini kuwa Johari kwa wazazi wake, pia kuwa lulu kwa jamii hatimaye kuwa
tunu ya taifa huku akitwaa taji la umalkia wa ulimwengu.
Sura
ya pili ni mwanamke mke. Ndiyo hapa namzungumzia mwanamke mke.
Hakuna mwanadamu ambaye ni mkamilifu lakini katika surah ii mwanamke anapaswa
kuwa muadilifu wa kupindukia, hapa anapaswa kuwa na hazina ya kutosha ya
hekima. Huku akimiliki bustani kubwa ya uvumilivu lakini hayo yote tisa, kumi
anapaswa kuvaa medali ya upendo moyoni. Kulingana na uzito wa surah ii,
mwanamke hapa anavaa majukumu mazito ya kumlea mumewe, kuwalea wanawe, kulea
ndugu lakini hapa anakuwa ni bawabu inayoumnganishwa nguzo za mlango na mlango
wenyewe. Lugha tamu yenye ukarimu iliyochanganyikana na upole ndiyo humfanya
mke kuwa mke bora yaani mke mwema. Kama mwanamke akiivaa surah ii barabara basi
dunia nzima itakuwa sawa na kijito kidogo kilichojificha na mharamia huku
samaki wakazi wakiwa katika furaha ya maisha.
Sura
ya tatu ni mwanamke mama. Hapana shaka kila mtu katika bongo
zake anaijua hii sura. Kwa kuwa baada a mtu kuolewa basi kifautacho ni mtu kuwa
mama. Hivyo mwanamke mke akitunukiwa ujauzito, akapewa kinga kisha akafanikiwa
kutoa kiumbe aitwaye binadamu salama kutoka katika tumbo lake na kumleta katika
mgongo wa dunia basi huwa mama. Uchungu wa mwana aujuae mama, kama hivi ndivyo
mamabo yalivyo basi sina shaka kuwa mwanamke akiwa mama lazima ajue majukumu
yake. Jukumu lenye uzito ni hili la malezi.Ukisikia mwanamke anamwita mwanwe
mbwa wewe, bila shaka mwanawe atakuwa mbwa ndogo na huyo mama ndiye mbwa
mkubwa. Basi mwanamke anapaswa kutambua ya kuwa kuwa mama siyo jambo la kubebwa
na kidole kidogo cha mkono. Unapokuwa mama tunajua utahakikisha kuwa familia
imekula imeshiba tena imekula vinono, pa iwe safi kwa mwili na tabia lakini
wewe ndiyo kiungo wa familia. Pia wewe ni mwalimu wa kwanza wa familia, wewe
ndiye mlezi na wewe ndiyo njia ya kukifikisha kizazi chako kwenye mikono
salama. Basi usihakikishe wanao wanakuwa na tabia mbovu maadili duni na utu
dhaifu.
Sura
ya nne ni mwanamke kiongozi. Baada ya kuwa mama wa
familia yaani kiongozi wa familia bila shaka hatua ifuatayo ni kuwa kiongozi na
si mtawala. Jane Radier ni mwanamke shupavu, jasiri mwenye kiremba cha uongozi
lakini name nimvishe joho la umalkia kwani yeye hutambua kwa kaisi kikubwa
nafasi ya mwanamke kama kiongozi na bila shaka ni moja kati ya kina Mama Samia
wa baadaye. Kujiheshimu kimavazi na kuwa na adabu ya mazungumzo, kuishi kwa
malengo, kuwa mwajibikaji, kujali muda hayo ni tisa na kumi ni kuwa na hofu ya
Mungu ndiyi kutamfanya mwanamke kuwa kiongozi bora. Sambamba na hayo mwanamke
lazima awe na uthubutu, kukubali kukoselewa nako ni sehemu ya nguzo zinazojenga
nyumba imara ya mwanamke kiongozi. Kwa kuwa alizungumza Jane mimi nisiwe mwenye
kutia chumvi zaidi kwani nikizidi kusherehesha nitakuwa mwathilika wa ile
methali ya Kiswahili isemayo mapishi mengi huharibu radha ya chakula au miruzi
mingi humpoteza mbwa hapo naweka nukta.
Sura
ya mwisho ni mwanamke bandia. Kwa nini uwe bandia?
Kwa nini usiwe halisia? Huu ni mtihani (mrundikano wa maswali) ambayo majibu
yake kila mtu anayo kwenye hifadhi ya bongo yake kichwani. Mwanamke hapaswi
kuvaa kama mwanamume, hapaswi kuwa na roho ya korosho (roho ya kwa nini).
Kuishi kwa kuiga siko kuzuri kwani mwishowe kutakuja kukushinda na kuibukia
kuwa kituko hatimaye kubaki kusema majito ni mjukuu. Mwanamke napaswa kuwa kama
kito cha dhahabu ghali king’aacho kila wakati na kinachovutia nyoyo na mato ya
watu wengi. Ukiishi vile unavyopaswa kuishi basi huna haja ya kung’anini kuketi
kiti kimoja na mwanaume. Acha mwanaume awe mwanaume na wewe uwe ulivyo.
Kutokana na sura hizo
tano za mwanamke bila shaka sasa kutakuwa na maswali machache. Lakini mwenye
kuelewa tayari atakuwa ameelewa ni wapi pa kuchagua, ni wapi pa kupuuza na ni
wapi pa kukimbilia. Mwanamke hapswi kukombolewa na shirika, asasi, taasisi wala
mdau yoyote bali anapaswa kujikomboa mwenyewe na kama atafauata misingi na
kanuni za maisha ya kike basi hutosikia katu suala la ukombozi wa mwanamke.
Wacha nafsi zijililie zenyewe ndiyo kauli inayofunga nayo kwa leo huku
nikikitaka binti wa kitanzania kuwa na vazi lako la kike linakutosha,
linakupendeza na dnilo litakalokultea heshima mbele za watu.
No comments