Header Ads

WAZIRI TIZEBA AIJIA JUU BODI YA KAHAWA


Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba ametaka sheria iliyounda Bodi ya Kahawa (TCB) iangaliwe upya ili chombo hicho kibebe jukumu la kusimamia uzalishaji kahawa.

Dk Tizeba amemtaka mwanasheria wa TCB, Engerasia Mongi kwenda Dar es Salaam mara moja, ili kushirikiana na wanasheria wa wizara kuanza mchakato wa kubadili sheria hiyo.

Waziri Tizeba alionyesha kukerwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo aliposema kwamba moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kusimamia sekta ya kahawa na sio uzalishaji.

Katika mazungumzo hayo ilibainika kuwa jukumu la kusimamia uzalishaji wa kahawa limeachwa kwa halmashauri za wilaya, ambazo kwa maoni ya waziri, zina mazao mengi ya kusimamia.

“Haileti afya. Kuna vacuum (ombwe) kubwa namna hii! Nataka tukubaliane suala la uzalishaji wa kahawa nchini halina mwenyewe. Halmashauri haziwezi kwa sababu zina mazao mengi,” alisema.

“Kama kazi yako ni ku monitor (kusimamia) tu maana yake you are not responsible (huwajibiki). Lingekuwa ni jukumu la bodi kungekuwa na kitengo kabisa cha uzalishaji Kahawa,” alisema.

“Mwanasheria nenda wizarani kamtafute mkurugenzi wa maendeleo ya mazao, mlete muswada Septemba hii ili tuiongezee bodi jukumu la kusimamia uzalishaji wa kahawa. “Kumbe hata pesa nimewaachia nyingi za nini kama hamsimamii kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa nchini?

“Nilikuwa najiuliza kwa nini uzalishaji wa kahawa uko stagnant (umedorora) kumbe haina mwenyewe! Tutabadilisha majukumu yenu. Huwezi kusimamia kitu hakipo,” alisema.

Waziri Tizeba alisema katika marekebisho hayo ya sheria namba 23 ya mwaka 2001, kama ilivyorekebishwa na Sheria ya Mazao namba 20 ya mwaka 2009, jukumu la uzalishaji liwe la kwanza.

Katika mazungumzo hayo na wafanyanyakazi na menejimenti ya bodi hiyo, Katibu Tawala (RAS) wa Mkoa Kilimanjaro, Aisha Amour alipendekeza sheria yote iliyounda bodi ipitiwe upya.

Awali, Kimaryo alisema majukumu ya bodi ni kusimamia sekta ya kahawa na kuratibu majukumu shirikishi ya wadau wa kahawa ikiwamo uzalishaji kahawa.

Akitembelea eneo la ushughulikiaji sampuli za kahawa, Dk Tizeba aliitaka bodi hiyo kutafuta dawa ya kudumu kudhibiti uvushaji wa kahawa kimagendo kwenda nchi jirani na kuitaka kutafuta njia bora za kuvifanya vyama vya ushirika mkoani Kagera, kununua kahawa kwa bei ya juu kama ile inayotolewa na kampuni za Uganda.

Inadaiwa mwaka 2015, tani 12,000 za kahawa zilisafirishwa kimagendo kupitia Kagera.

No comments

Powered by Blogger.