Header Ads

SHAIRI: PAMBANA NA HALI YAKO

PAMBANA NA HALI YAKO
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

Ninakamilisha malengo, wewe baki na umbea,
Nitainua mjengo, wewe kwenu umekaa,
Kuimba imba boringo, wewe baki kuongea,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Umekuwa shilawadu, shirika lako umbea,
Umeshakuwa mdudu, sumu yako inaua,
Hasidi una husudu, wewe chuki kila saa,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Kazi kuchagua kazi, eti maisha magumu,
Chakula chako viazi, vya chipsi siyo vitamu,
Umewekeza mavazi, na kubadilisha simu,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Mwanaume unabeti, kutwa unashinda gym,
Stori zako za mabinti, kutafuta tu madem,
Mwanaume hutafuti, kazi yako kulaum,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Unalia na serikali, eti haikupi ajira,
Wewe hutaki shughuli, hata za kibiashara,
Elimu yako  kivuli, ya kuwaza mishahara,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Thamani ya mwanamke, wewe dada huijui,
Umekaa teketeke, utuchune kama chui,
Shukran ni mateke, ya punda kama hujui,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Unashinda umelala, kama mbuzi wa kigeni,
Vya nyumbani unakula, kama nzi na kunguni,
Amka katafute hela, hela haziji nyumbani,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Kazi ni kucheka cheka,, kusifia vya wenzako,
Wewe lini utatoka, uwe kama baba yako,
Jambo zuri ukitaka, nenda katafute vyako,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Unawaza tu ushenzi, na starehe za dunia,
Unaendekeza mapenzi, kuku bata disco bia,
Kuchat kwako ni kazi, na movie za kikorea,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Nikikesha darasani, napiga zangu msuli,
Kinakuuma moyoni, wanisema kwa kejeli,
Wenzako wapo chuoni, huku wewe umefeli,
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi

Unataka sifa kwako, hutaki ziwe wenzako,
Kila kizuri chako, gari la shangazi yako,
Mjengo wa baba yako, zipo wapi mali zako?
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Nilipochumia juani, uliniona kama nyani,
Leo nipo kivulini, sasa chuki ni ya nini?
Ninajiona kama nini, kwani wewe hujioni?
Pambana na hali yako, yangu niachie mimi.

Na Shablil President.
Wa Nyamwezi Kingdom.
2017 Kamilisha Malengo.
0718526159/0763902318.

No comments

Powered by Blogger.