Header Ads

MUME MWEMA
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA
Naongea na Felister, mwambie naye Mwajuma,
Naongea na Calister, mwambie naye Fatuma,
Ninaongea na Ester, mwambie naye Rehema,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Kimfacho mtu chake, shetani mbuyu wake,
Kila mtu ana wake, kila kitu kina chake,
Kuna sifa kuwa mke, msikie wanawake,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Mume mwema ni zawadi, maishani ni silaha,
Mtafute kwa juhudi, wa ubani wa furaha,
Usifanye rimradi, mtafute kwayo staha,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Mume mwema siyo mali, kutazama yake hali,
Mume mwema siyo mwili, kupangika kama reli,
Mume mwema ni akili, dada huo ndo ukweli,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Ukipenda mwenye hela, utampata msela,
Penzi likufunge jela, kama Wema na Kajala,
Utageuzwa jalala, hutokula hutolala,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza Tltafakuri.

Mume mwema siyo nguo, kuuzwa Kariakoo,
Mume mwema ni funguo, peponi upande cheo,
Mume mwema ni chaguo, fasaha mwenye upeo,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Mume mwema ni Baraka, mtemi kama Ngeleja,
Mume mwema ni Kiraka, Zambi Shaban wa haja,
Kusaga sipomtaka, basi utampata teja,
Ukitaka Mume Mwema, fanya kwanza tafakuri.

Ifanye dua uombe, mume atoke kwa Mungu,
Waganga sinywe kikombe, fitina ya ulimwengu,
Usome huu ujumbe, upokee dada yangu,
Ukitaka Mume Mwema, fanya kwanza tafakuri.

Mume siyo sharobaro, wala siye barobaro,
Si yule wa kigodoro, hatokei uchochoro,
Siyo yule wa miparo, asiwe nyingi kasoro,
Ukitaka nume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Mzuri umpendaye, tena awe Mcha Mungu,
Maadili ajuaye, wa huruma mlimwengu,
Mahaba ayajuaye, mpokee dada yangu,
Ukitaka mume mwema, fanya kwanza tafakuri.

Na Shablil President
Wa Nyamwezi Kingdom
2017 Kamilisha Malengo
0718526159/0763902318

No comments

Powered by Blogger.