DARASA LA NJE YA DARASA
Darasa ni darasa, darasa
ni ukurasa, sina budi kuunasa, kama darasa la anasa hilo ndilo darsa linalotutesa
lakini kitu cha kutambua ni kwamba darasa la nje ya darasa ni muhimu kuliko darasa
la ndani ya darasa. Je darasa la ndani
ya darasa ni nini hasa?
Basi mwanagenzi wa Kisiwa
cha Kiswahili hili leo naomba tutete kidogo juu ya umuhimu wa darasa. Tumezoea
kusikia ya kuwa wazee wetu hasa wale tunaowaita wahenga ni wajuvi sana wa
busara tena wana utajiri mkubwa wa maadili, ndipo hapo tunapata wasaa wa kusema
ya kuwa ya kale ni dhahabu, na palipo na wazee haliharibiki jambo.
Siki hizi utamaduni wa
Bwana Koloni yaani huyu mzungu aliyetufundisha ushenzi akatuletea ujinga na
sasa ametuangamiza katika janga kubwa janga linatutafuna sisi na vizazi vyetu.
Sisemi kuwa hakuna matunda matamu yenye virutubisho tuliyovuna kutoka kwake la
hasha! Yapo tena yapo mengi sana.
Natafakari hapa kwa kuona
jinsi alivyotuletea elimu ya kukaa darasani, huenda sina weledi wa kuweza
kugundua siri iliyomo ndani ya maudhui ya elimu yake lakini kila nikiona wale
wanaojinasibu kuwa wameelimika ndio hao hasa huonekana kama waliopotoka katika
jamii yetu ya nchi ya rutuba wa uoto wa kijani.
Tazama jinsi wanafunzi wa
usasa wanaojinasibu kuwa wamepata elimu yao darasani tena lile darasa la
koloni, jinsi wanavyovaa, jinsi wanavyootembea, jinsi wanavyozungumza na jinsi
wanavyoigiza maisha badala ya kuishi maisha halisi. Leo hii wamekuwa ni watu wa
ajabu, watu wa kumtupa Mungu si wale wa kumpokea Mungu. Swali langu ni kuwa elimu
yao imewafunza nini? Leo maisha ya kijirani yapo hatarani, maisha ya kusaidiana
yapo kwenye kaa la moto hata salamu sasa imekuwa kama shilingi inayochezewa
karibu na tundu la choo.
Najiuliza sasa hivi
ulimwengu umehamia kiganjani. Hivi ni Kiganjani? Aah ndiyo kwani ndipo hasa
skanu zinapoishi, kuna rafiki yangu aliwahi kuniuliza habari za skanu
nikamwambia ndiyo hizo wanaita Smartphone. Ndizo hasa zimefikia hatua ya
kuifanya dunia hii ikaitwa kijiji ha ha ha yaani leo ulimwengu wa Mungu umekuwa
sawa Kijijini kwetu Ibambo kama haileti maana basi italeta laana.
Sasa hii elimu inayofunza
watu watu zinaa, inafunza watu wizi tena wizi wa mali za umma, kuibia
wasakatonge kina Chiku na Kapili waliolelewa kimasikini, elimu inayomfanya mtu
amsahau baba mbaya zaidi wanamsahau hadi mama aliyewabeba tumboni kwa miezi
tisa, haya ni majonzi makubwa.
Labda niseme tu tatizo
siyo elimu lakini ni elimu ya darasani yaani ndani ya darasa, lakini je, vipi
kuhusu elimu ya nje ya darasa?
Waswahili tuna misemo
bwana mathalani huu wa usiache mbachao kwa msala ulipatao. Yaani leo sayansi na
teknolojia ya Bwana Koloni ndiyo imegeuka msala, msala wenye kupita. Vipi
kuhusu zile adili za Mtemi Mirambo, vipi kuhusu zile nasaha za Chifu Mkwawa.
Tazama leo zimekuwa mbachao na watu wanaziacha.
Ninachokifahamu mimi
kuhusu elimu ya nje ya darasa. Elimu inayotufunza kuvaa vema, elimu
inayotufunza kusalimu kila mtu, elimu inayotunabaishia maisha ya kijirani.
Ubinanadamnu ni huruma bwana. Utu ni upendo. Utaifa ni uzalendo, lakini yako
wapi haya leo?
Kizazi kimekuwa hayawani
yaani kilichokosa haya, leo mzee wa kaya ndiye hasa anatukuza umalaya. Kizazi
kimekuwa kizazi kilichopotea. Kimetumbukia kwenye korongo kimezama mtoni ona hata
hakielei baharani.
Sasa wanagenzi mwenzangu
waswahili husema kusema sana si kumaliza, lakini ubora wa mzuingumzaji ni yule
mwenye kuzungumza kwa uchache wenye busara. Basi nami nikhitimkishe kwa kusema
kuwa ni muhimu kupata elimu ya nje ya darasa ile elimu unayotolewa na mjomba,
shangazi, jirani baba na pengine hata mama elimu Ya nje ya darasa.
……………………………………………………………………………………………………
No comments