Header Ads

SHAIRI: WACHAWI WADAKWA WAKIWA KIWENYE KIKAO CHA MAANGAMIZI.

Image may contain: one or more people, people sitting and outdoor





KIKAO CHA WACHAWI
SHAABAN MAULIDI
TABORA TANZANIA

🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥

Nani kasema uchawi, eti uchawi haupo,
Nimeuona uchawi, uchawi jamani upo,
Wachawi wenye uchawi, wachawi jamani wapo,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Nimeona baharini, waketi juu ya maji,
Tena wapo kikaoni, kikao cha upangaji,
Wanaishi duniani, nyikani na kwenye miji,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Sura zao ni nyeusi, machoni wawaka moto,
Nguo zao ni nyepesi, zafusha mpaka mato,
Maneno yao risasi, yaua hadi watoto,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Mwenyekiti wao Ghoshi, kichwani kaota pembe,
Anafuka tu moshi, mkia kama wa ng'ombe,
Ana bawa la kizushi, meno yake kama jembe,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Ana sauti ya radi, sauti iliyo chungu,
Aongea kwa midadi, na mikono kama rungu,
Ni mganga fundi jadi, kinywani ana ukungu,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Ghalfa nikaona giza, mara moshi ukafukiza,
Ikaanza miujiza, nikahisi makengeza,
Mara Ghoshi kaagiza, amri ya kuangamiza,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Wajumbe kumi na nane, wachawi hawa ajabu,
Waume wapo wanane, vikongwe tena vibabu,
Wakike wapo wanne, vibibi vyenye sharubu,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Wachawi hawa tajiri, japo hawaonekani,
Mahekalu ya kifahari, wameyaficha majini,
Wana ndege na magari, yakupaa tu angani,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Tena wanayo mapesa, mapesa yao haramu,
Vizuu wanavitesa, na kuvinyonya damu,
Wachawi nazo anasa, ni walevi wa chapumu,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Wao wamejizindika, kwa tunguli na hirizi,
Kijiji wamekiteka, watu ng'ombe na mbuzi,
Uchawi wameushika, kuwapoka hatuwezi,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Mipango yao kuua, pamoja kunyonya damu,
Usiku kutuchukua, kufanya kazi kwa zamu,
Akili wametutoa, bongo zetu si timamu,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Wanakula nyama mbichi, na damu za wanadamu,
Uchawi hawauachi, kuua kwao karamu,
Wana maji wana nchi, wanawanga kwa awamu,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Hawana hata huruma, hawa wachawi wabaya,
Hawana hata heshima, tabia zao ni mbaya,
Wameua kina mama, na kina baba vibaya,
Nimewaona wachawi, wameketi kikaoni. 


Sasa nimeshawaona, nawatafutia dawa,
Dawa yao ya kisuna, matunguli kutobowa,
Nimetoa kupambana, mimi ndiyo mtolewa,
Nimewaona wachawi, wameketi Kikaoni. 


Usikose sehemu ya pili...

Na Shablil President
Wa Nyamwezi Kingdom
2017 Kamil Isha Malengo
0718526159/0763902318

No comments

Powered by Blogger.